Linapokuja swala zima la kununua smartphone au simu ni wazi kuwa unahitaji simu ambayo utaweza kutumia hata baada ya miaka mitatu mbeleni, baadhi ya watu hufanya makosa ya kununua simu ambazo hazina baadhi ya sifa hivyo kujikuta wakibadilisha simu kila baada ya mwaka mmoja au hata miezi sita.
Kuliona hili nimekuletea makala ambayo naamini itaweza kusaidia kupata simu bora sana kwa kuangazia baadhi ya vitu muhimu vya kuangalia kabla ya kununua simu na kama kwa namna yoyote vitu hivi havipo basi ni muhimu sana kuangalia machaguo mengine yenye sifa hizi.
Bila kupoteza muda twende moja kwa moja tuangalie vitu ambayo kama havipo kwenye simu yako unayotaka kununua basi ni bora kuangalia machaguo mengine ili kuwa na simu yenye sifa bora.
TABLE OF CONTENTS
Haina Sehemu au Uwezo wa eSim

Ni Wazi kuwa sim card zinaenda zikipotea na kadri muda unavyozidi kwenda ni wazi kuwa unahitaji simu yenye uwezo wa kusupport eSim. Kama hujui eSim ni nini unaweza kusoma makala yetu hapa kujua jinsi eSim inavyofanya kazi.
Kwa ufupi, eSim ni laini za kidigitali ambazo zinaweza kutumika kwenye simu bila kuwa na laini ile ya plastick ambayo ni lazima uweke kwenye simu. simu yenye eSim inaweza kuhifadhi laini zaidi ya moja na pia unaweza kuhamisha kutoka simu moja kwenda nyingine kwa urahisi kwa kutumia QR Code. Kwa sasa huduma za eSim zinapatikana kwenye mitandao karibia yote Tanzania na kwa gharama nafuu unaweza kubadilisha line yako ya plastiki kuwa eSim.
Hivyo basi, kama simu yako haina sehemu ya eSim basi ni wakati wa kufikiria sana kutafuta simu yenye uwezo huu, na kama unatafuta kununua simu kwa sasa basi usinunue simu ambayo haina sehemu hii ya eSIM ambayo ni muhimu sana kwa sasa.
Ina Uhifadhi wa Ndani Chini ya GB 128 (Internal Storage)

Ni muhimu sana kuhakikisha uwezo wa ndani wa simu yako una support angalau kuanzia GB 128, kadri muda unvyozidi kwenda simu zenye uwezo wa GB 64 na kushuka chini zina kuwa na uwezo mdogo sana wa kuweza kuendesha apps nyingi ambazo kwa sasa zinaonekana kuhitaji uwezo zaidi. Kwa mfano app ya Instagram na WhatsApp tu kwa sasa zinachukua nafasi zaidi ya MB 900+ kila moja.
Unaweza kusema kwa kuwa simu yako ina nafasi ya kuweka Memory Card basi hakuna shida, HAPANA uwezo wa uhifadhi wa ndani (Internal Storage) na uhifadhi wa kuongeza kwa memory card ni tofauti kabisa, kuanzia uharaka wa kuandika data na hata uwezo wa apps kuhifadhi data. Hii ni kwa sababu apps nyingi huweza kuchagua kutumia uwezo wa ndani kuliko kutumia Memory Card kuhifadhi data hii ni kwa sababu za muundo wa app na hata usalama wa data zako kwenye app husika.
Hata hivyo simu nyingi zenye storage chini ya GB 128 nyingi pia zina kuwa na uwezo mdogo wa RAM hivyo hufanya simu kuwa nzito kutumia. Hivyo basi kama unataka simu itakayo endana na wakati na yenye uwezo bora ni vyema kuhakikisha hununui simu yenye storage chini GB 128.
Inayo Battery Ndogo chini ya 5000 mAh

Kama kwa sasa unatumia simu ya Android ambayo inakuja na battery yenye uwezo mdogo chini ya 5000 mAh basi ni wazi kuwa unahitaji simu yenye uwezo mkubwa zaidi. Kwa upande wa iPhone hakikisha simu yako inakuja na mfumo mpya wa iOS kwani kama simu yako inakuja na battery ndogo na inatumia mfumo wa iOS wazamani basi lazima utaona simu yako inaisha chaji kwa haraka.
Ni muhimu kujua kuwa kuna utofauti mkubwa wa utumiaji wa chaji kati ya simu za iPhone na Android, Simu za iPhone huja na mfumo maalum wa kusaidia simu kutotumia chaji kwa kiwango kikubwa kutokana na kuwa Apple kutengeneza vifaa vyote wenyewe kuanzia memory, chipset na vingine. Japo kuwa mfumo wa Android nao pia unakuja na uwezo huu lakini kwa Android ni lazima battery kuwa na uwezo mkubwa ya mAh kubwa kutoka na vifaa mbalimbali vya simu hizi hutengenezwa na makampuni mbalimbali hivyo ni ngumu kuweza kudhibiti uwezo wa kutumia chaji kwa baadhi ya vifaa.
Mfumo wa Zamani Sana wa Uendeshaji

Kama unatumia Android hakikisha simu yako inaweza kutumia mfumo wa Android kuanzia Android 13 na kuendelea kwa watumiaji wa simu za iPhone hakikisha simu yako inakubali mfumo mpya wa iOS 17 na kuendelea hii ina maana kuwa simu yako itaendelea kufanyakazi hata kwenye apps bora za kisasa ambazo zitakuwa zinazinduliwa. Ni muhimu sana kuwa makini na kuzingatia simu ilitoka na mfumo upi wa uendeshaji, kwa kuangalia hili utaweza kujua simu itapokea mifumo mingapi ya uendeshaji kuanzia ilipotoka.
Haina Viunganishi (USB Type C)

Hakikisha simu yako inakuja na viunganishi vya kisasa, kwa mfano upande wa bluetooth hakikisha simu yako inayo bluetooth kuanzia 5.0 na kwa upande wa USB hakikisha simu yako inatumia mfumo mpya wa USB Type C, Hii itakusaidia sana kwenda na wakati na utaweza kuunganisha vifaa vingi ambayo vinaendana na teknolojia hizi.
Haina Network ya 5G

Mwisho kabisa ningependa kuongelea kuhusu Network, kama unataka kuhakikisha unatumia simu yako kwa muda mrefu sana bila kubadilisha hakikisha simu yako inakuja na mfumo wa Network wa 5G, hii itakusaidia sana kwani simu yako itakuwa ime endana na wakati kwa kiasi kikubwa. Japo kuwa hili sio la muhimu ila litakusaidia sana pale utakapo hitaji kutumia mfumo wa 5G kwenye simu yako.
Hitimisho
Kwa kuangalia vitu hivi na uhakika utapa simu yenye sifa bora na yenye kwendana na wakati, hata hivyo simu nyingi zenye sifa hizi huwa ni simu bora kuanzia simu za daraja la kati hadi simu za daraja la juu hivyo lazima utapa simu yenye uwezo bora hata kwa sehemu nyingine zilizobaki ambazo sio muhimu sana. Kama unatafuta simu unaweza kutembelea Tanzania Tech Gadgets kupitia hapa, kama una maoni au ushauri unaweza kuandika kupitia sehemu ya maoni hapo chini.
