Google imetangaza rasmi kuingia sokoni kwa simu yake mpya ya daraja la kati, Google Pixel 10A. Simu hii inakuja kama mrithi wa Pixel 9a, ikiendeleza utamaduni wa Google wa kutoa simu zenye uwezo mkubwa wa kamera na programu (software) kwa bei nafuu kulinganishwa na simu zao za daraja la juu.
Hata hivyo, tofauti na matoleo ya miaka iliyopita, Pixel 10A imeibua mjadala mkubwa kutokana na kufanana kwake kwa kiasi kikubwa na toleo la Pixel 9a, huku maboresho yakiwa machache sana.
TABLE OF CONTENTS
Muundo na Kioo (Design & Display)
Kwa upande wa muonekano, ni vigumu kutofautisha Pixel 10A na Pixel 9a. Simu hii imebaki na umbo bapa lenye kingo za aluminiamu na sehemu ya nyuma ikiendelea kuwa plastiki badala ya kioo.
Kioo chake ni cha inchi 6.3 (Actua Display) chenye refresh rate ya kuanzia 60Hz hadi 120Hz. Hata hivyo, Google wamefanya maboresho kidogo kwenye ung’avu (brightness), ambapo kioo cha Pixel 10A kinaweza kufikia nits 3,000, likiwa ni ongezeko la asilimia 10 kulinganishwa na toleo la nyuma la Pixel 9A. Vilevile, kioo hicho sasa kinalindwa na teknolojia mpya ya Gorilla Glass 7i, ambayo ni imara zaidi dhidi ya mikwaruzo. Kwa upande wa rangi mpya zilizotambulishwa kwenye toleo hili ni Fog, Obsidian, Berry, na Lavender.
Utendaji na Sifa za Ndani (Performance)
Katika hatua isiyo ya kawaida, Google imeamua kutumia chipset ya mwaka jana, Tensor G4, badala ya kuweka toleo jipya la Tensor G5 ambalo linapatikana kwenye simu za Pixel 10 za daraja la juu. Hii inamaanisha kuwa kiutendaji, Pixel 10A ina nguvu sawa kabisa na Pixel 9a.
Sifa nyingine za msingi zimebaki vilevile:
-
RAM: 8GB
-
Uhifadhi wa Ndani (Storage): Inaanza na 128GB
-
Betri: 5100 mAh
Maboresho madogo yamefanyika kwenye mfumo wa kuchaji, ambapo sasa inaweza kuchajiwa kwa waya kwa kasi ya wati 30 (ikilinganishwa na wati 23 za awali kwenye pixel 9A) na kuchaji bila waya (wireless charging) kwa wati 10.
Kamera na Programu
Eneo ambalo Google huongoza siku zote ni kwenye kamera, na Pixel 10A haijawa nyuma, ingawa vifaa vyake vya kamera (hardware) havijabadilika. Simu ina kuja na kamera mbili huku kamera kuu ikiwa na 48MP na nyingine ya ultrawide ikiwa na Megapixel 13MP.
Nguvu kubwa ya simu hii ipo kwenye akili mnemba (AI) na programu. Inakuja na vipengele kama “Auto Best Take” ambayo hurekebisha nyuso kwenye picha za pamoja ili kila mtu aonekane vizuri, na “Camera Coach” inayomsaidia mtumiaji kupiga picha bora.
Aidha, simu hii inakuja na ahadi ya miaka 7 ya sasisho za mfumo wa Android na ulinzi (security updates), jambo linaloifanya kuwa simu inayoweza kutumika kwa muda mrefu bila kupitwa na wakati.

Bei na Upatikanaji
Google Pixel 10A imezinduliwa kwa bei ile ile ya kuanzia $499 (kama TZS 1,350,000 hivi kabla ya kodi).
Kwa ujumla, Pixel 10A inatazamwa kama simu nzuri kwa mtu anayetaka kuingia kwenye mfumo wa Google Pixel kwa mara ya kwanza au anayetoka kwenye simu za zamani sana (kama Pixel 6a au 7a). Hata hivyo, kwa watumiaji wa Pixel 8a au 9a, hakuna sababu kubwa ya msingi ya kubadili simu na kuhamia toleo hili jipya.

