Kama wewe ni mmoja wa watumiaji wa mtandao wa WhatsApp basi habari njema ni kuwa kampuni hiyo siku ya Jumatano imeanza kuachia rasmi sehemu mpya ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu, sehemu inayokupa uwezo wa kupanga muda wa kutuma meseji (schedule messages) kwenye chat za kawaida na hata kwenye magroup.

Sehemu hii mpya imeanza kuwafikia watumiaji wote duniani kote wanaotumia simu za Android pamoja na iOS. Mara tu sehemu hii itakapofika kwenye simu yako, utaweza kuandika meseji yako kama kawaida kisha unabofya na kushikilia kwa muda (long-press) kitufe cha kutuma (send) ili kuchagua muda unaotaka meseji hiyo itumwe. Unaweza kupanga meseji itumwe kuanzia dakika 10 zijazo hadi siku 14 mbele.
Pia, watumiaji wataweza kuona meseji zote walizozipangia muda wa kutumwa na kuzifuta pale wanapohitaji kufanya hivyo. Hata hivyo, bado haijawekwa wazi kama kutakuwa na uwezo wa kubadilisha muda wa meseji ambayo tayari imeshapangiwa muda.
Kitu kizuri zaidi kuhusu sehemu hii ni kuwa meseji ulizozipangia muda zitatumwa hata kama simu yako itakuwa imezimwa au haina mtandao (internet) wakati huo ukifika. Vilevile, unaweza kupanga muda wa kutuma meseji za maandishi, picha, na hata video.
Sehemu hii inaweza kuwa msaada mkubwa sana hasa pale unapotaka kumtakia mtu heri ya siku ya kuzaliwa kwa wakati sahihi au unapo chat na watu waliopo nchi zenye tofauti kubwa ya masaa. Pia wafanyabiashara wataona urahisi wa kupanga meseji na taarifa kwa wateja wao, huku wale wanaotumia WhatsApp kupanga kazi wakiweza kutuma taarifa kwa timu zao kwa muda maalum.
Ikumbukwe kuwa mitandao shindani ya WhatsApp kama vile Telegram na Signal tayari ilikuwa na uwezo huu wa kupanga muda wa kutuma meseji kwa muda mrefu, hivyo WhatsApp inayomilikiwa na kampuni ya Meta imechelewa kidogo kuleta sehemu hii.
Kama bado hujaona sehemu hii kwenye simu yako hakikisha una update programu yako ya WhatsApp kupitia Play Store au App Store. Unaweza kutuambia maoni yako kuhusu sehemu hii mpya kupitia sehemu ya maoni hapo chini