Kama wewe ni mmoja wa watu ambao wanatumia mtandao wa Adsense kwa ajili ya kutengeneza pesa mtandaoni basi ni wazi una taarifa muhimu ya uhitaji wa kuweka TIN Number au namba ya utambulisho wa mlipa kodi kwenye akaunti yako ya Google Adsense kwa hapa Tanzania.
Kama kwa namna yoyote huna taarifa hizi basi kupitia makala hii nitakujuza kuhusu sheria hiyo mpya ya Google Adsense, pamoja na jinsi ya kukamilisha hatua hizi ili kuendelea kutengeneza pesa kupitia Adsense ukiwa mlipa kodi halali kwenye taifa lako.
Kwa mujibu wa Google hivi sasa ili kuendelea kutengeneza pesa kupitia Huduma za Google hii ikiwa ni pamoja na YouTube, Blogs zenye Kuonyesha matangazo ya Google Adsense, Apps na huduma nyingine za Google ni lazima uwe mlipakodi halali wa Tanzania hivyo ni lazima kuwa na TIN Number.
Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Google, Sheria ya Tanzania inataka Google kuzuia kodi kwenye malipo fulani ambayo Google inakulipa wewe na kutoa taarifa za malipo hayo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, malipo yanayofanyiwa makato ni yale yanayohusiana na maudhui ya kidijitali, kama vile video za YouTube, programu za Play, malipo ya AdSense, na kadhalika. Makato haya yanafanywa kwa mpokeaji wa malipo aliye Tanzania kwa kiwango cha asilimia 5% ya jumla au sehemu ya mapato anayostahili kimkataba, bila kujali ada za huduma au kodi nyingine zilizokwisha katwa.
Kila mwezi Google inatakiwa kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, taarifa ambazo ni pamoja na:
- Malipo ya jumla yanayostahili kukatwa kodi ya Tanzania.
- Jumla ya kiasi kilichokatwa
- Namba yako ya utambulisho wa mlipa kodi
- Anwani yako, na aina ya malipo, kwa mfano, malipo ya maudhui ya kidijitali.
Kuweka TIN Number Kwenye Akaunti ya Google Adsense
Ili kuhakikisha unaendelea kupokea malipo yako unatakiwa kuweka Number ya TIN yako kupitia kwenye ukurasa maalum wa malipo kupitia Google, unatakiwa kuweka namba yako ya utambulisho wa mlipa kodi, na upakie Hati ya Usajili ya Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA. Kwa maelezo zaidi ya jinsi ya kuwasilisha taarifa zako za kodi, angalia makala hii.
Kwa kufuata hatua hizi natumaini utakuwa umeweza kuweka namba yako ya utambulisho wa mlipa kodi kupitia akaunti yako ya Google Adsense. Kama unataka kujua jinsi ya kupata TIN Number online unaweza kusoma hatua hizo hapa.