in

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Ian Ferrao Astaafu

Nafasi ya Ferrao itachukuliwa na anayetokea kampuni ya Safaricom ya Kenya

Mkurugenzi mtendaji wa Vodacom Ian Ferrao
Ian Ferrao (kushoto)

Taarifa kutoka kwenye mtandao wa mwananchi hapo jana zinasema kuwa, Mkurugenzi mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao ametangaza kuachia mikoba ya kuiongoza kampuni hiyo baada ya mkataba wake kufika tamani.

Kutokana na hilo, Ferrao atakabidhi majukumu kwa mrithi wake, Sylvia Mulinge kuanzia Juni Mosi mwaka huu na kuhitimisha miaka mitatu ya kuiongoza kampuni hiyo inayoongoza kwa idadi kubwa ya wateja nchini. Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa bodi ya Vodacom, Ali Mufuruki inaeleza makabidhiano ya ofisi kati ya Ferrao na Sylivia yatafanyika kwa miezi mitatu na kukamilika rasmi Agosti 31 mwaka huu 2018.

Nafasi ya Ferrao itachukuliwa na anayetokea kampuni ya Safaricom ya Kenya ambako kwa sasa anafanya kazi kama mkurugenzi wa Huduma kwa wateja aliyojiunga nayo tangu mwaka 2006. Akizungumzia kuondoka kwa Ferao jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Vodacom, Ali Mufuruki alimpongeza kwa kuiendesha kampuni hiyo kwa mafanikio tangu alipojiunga nayo mwaka 2015.

Kabla ya kujiunga na Vodacom Tanzania, Ferrao alikuwa mkurugenzi mtendaji wa Vodacom nchini Lesotho. “Ilikuwa ni nafasi adhimu kuiongoza Vodacom Tanzania katika kipindi cha mabadiliko na ukuaji. Najisikia fahari kufanya kazi Tanzania na kusaidia kuipeleka katika ulimwengu wa kidigiti na mabadiliko ya teknolojia,” alisema Ferrao.

Njia Mpya ya Kutengeneza Pesa Kupitia YouTube Shorts Video

Licha ya Vodacom Tanzania kufanikiwa kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake DSE zenye thamani ya Sh476 bilioni na kuwavuta zaidi ya wawekezaji 40,000 wa ndani, tayari kampuni hiyo imelipa gawio la Sh28.5 bilioni. “Sera ya gawio inataka walau asilimia 50 ya faida iliyopatikana itolewe kwa wanahisa lakini Vodacom imelipa asilimia 60,” inasema taarifa hiyo.

Mwenyekiti wa bodi alimtakia kila la heri Ferrao na kumkaribisha mkurugenzi mpya atakayeiongoza Vodacom kuwahudumia Watanzania kwa kuanzia Juni Mosi. “Tunamtakia heri Ferrao na familia yake maisha mema. Naomba kumkaribisha mtendaji mkuu mpya ambaye nina uhakika atafanya kazi na timu ya Vodacom na tutafurahia mafanikio siku zijazo,” alisema Mufuruki.

Written by Amani Joseph

Tanzania Tech tumejikita kuhakikisha hupitwi na habari yoyote ya teknolojia, endelea kuwa nasi tufuate kwenye mitandao ya kijamii.

Toa Maoni Hapa

Kumbuka ni Muhimu Kuandika Jina Halisi na Barua Pepe, Vigezo na Masharti Kuzingatiwa.

    Back to Top
    close