WhatsApp imetangaza kipengele muhimu kwa ajili ya sehemu ya Chaneli zake ili kunufaisha biashara, na waandaaji wa maudhui.
Katika toleo la hivi karibuni, kampuni hiyo inaanza kutoa uwezo mpya wa “subscriptions” (usajili wa kulipia). Kwa sasa, huduma hii inapatikana kwa baadhi ya watumiaji wa Android wanaojaribu toleo la beta.
Toleo la beta la WhatsApp la Android 2.25.19.3 linaonyesha nyongeza mpya kwenye programu hiyo ya WhatsApp, inayoitwa “Channel Subscriptions” (Usajili wa Chaneli). Kutokana na jina lenyewe, kipengele hiki kitawawezesha watumiaji kujiandikisha kwenye chaneli wanayoipenda na kulipia ili waweze kufikia maudhui maalum (exclusive content).
Chaneli ambazo zimejiandikisha zitaonyesha alama ya almasi kwenye sehemu ya juu ya programu kuashiria maudhui yao maalum. Kipengele hiki kinalenga hasa kuwaunganisha kwa undani zaidi waundaji wa maudhui na biashara na wateja wao na kuzalisha mapato kwa ufanisi.
Aidha, kupitia WhatsApp wamiliki wa chaneli wata takiwa kuthibitisha utambulisho wao kwa kuingia kwenye akaunti zao za Facebook ili kuweka malipo na miamala ya watumiaji salama.
Baada ya uthibitisho wa utambulisho, WhatsApp itaidhinisha maombi, na chaneli inaweza kutumika kama chaneli ya kulipia, ikitoa jumbe za kipekee, hadithi, na media kwa wafuasi wanaolipa.
Watumiaji wanaweza kujiandikisha moja kwa moja kwa chaneli ya kulipia kupitia WhatsApp, ikiwa pamoja na kuchagua mpango wao, na kuendelea na malipo.