Raila Odinga Kuishtaki Facebook na Cambridge Analytica

Raila naye kuishtaki kampuni ya Facebook sababu ya Cambridge Analytica
Raila Odinga Raila Odinga

Sakata la Facebook na kampuni ya Cambridge Analytica bado linaendela na wiki hii Facebook imeanza kuchunguzwa rasmi na FTC au (Federal Trade Commission) Shirikisho la Tume ya Biashara nchini Marekani. Wakati Facebook ikiendelea kuwa na siku mbaya kila siku.

Kinara wa upinzani Raila Odinga naye ameibuka na kusema ataushtaki mtandao wa Facebook pamoja na kampuni ya Cambridge Analytica kwa kutumia jina lake kuendesha kampeni ya kuchochea uhasama wa kikabila kwa lengo la kuhujumu azma yake ya kuwa rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017.

Akiongea na kituo cha Channel 4 News, Bw Odinga alisema kanda za video zilizosambazwa na Cambridge Analytica katika mitandao ya Facebook wakati wa kampeni zilimbandika sifa za ‘shetani muovu’ na zililenga kumharibia jina.

Advertisement

“Nilitamaushwa sana na hatua ya Facebook kukubali mtandao wao kutumiwa kwa njia za ukora. Nilikasirika sana na tunaendelea na mipango ya kushtaki Facebook..tutatumia mawiliki wetu nchini na wale wako nje ya Kenya,” alisema Bw Odinga.

Waziri huyo Mkuu wa zamani alikuwa anazungumza kwa mara ya kwanza tangu kufichuka kwa sakata kuhusu kampuni ya Cambridge Analytica kutumia habari za kibinafasi za watumiaji wa Facebook kuvuruga uchaguzi nchini Amerika na Kenya. Bw Odinga alisema kampuni hiyo ilitumia mwanya wa idadi kubwa ya Wakenya wanaotumia intaneti kusambaza propaganda za kisiasa.

“Kanda ya ‘The Real Raila Odinga’ ilionyesha kuwa Raila ni mtu mwovu..katili mwenyewe,” alisema Bw Odinga. Ripoti ya kampuni ya Privacy International ilisema kanda hizo ya ‘The Real Raila’ ambazo zilimuonyesha Bw Odinga kuwa mpenda vita na asiyepaswa kukubaliwa kuongoza, ziliundwa na shirika la Harris Media.

Katika mahojiano hayo, Bw Odinga alisema Harris Media na Cambridge Analytical ni mamoja.

Azma ya kazi ya Cambridge Analytica na Harris Media ilifadhiliwa na mteja mmoja na ililenga kutoa taswira mbaya katika kampeni. Ufichuzi wa Kituo cha Channel 4 uliotolewa wiki iliyopita ulifichua kanda ya kampuni hiyo ikijigamba jinsi ilivyounda upya chama cha Jubilee mara mbili na kukiandikia manifesto, kukifanyia utafiti wa kisiasa pamoja na kukiandikia hotuba zake.

“Tulitumiwa kama majaribio katika uchaguzi wa 2013 na hatukujua jinsi ya kukabiliana na hali hiyo. Walirudi tena 2016 na raundi hii walirejea na ujuzi wa juu sana wa kuvuruga kampeni za kisiasa mitandaoni,” alielezea Bw Odinga.

Baada ya kufichuka kwa sakata hiyo, kampuni ya Cambridge Analytica ilimtimua Mkurugenzi wake Mkuu Alexander Nix, kwa tuhuma za kushindwa kulinda sera za kimaadili za kampuni hiyo.

Chama cha Jubilee kilikanusha madai ya kushirikiana na kampuni hiyo lakini naibu mwenyekiti wa chama hicho David Murathe, alikiri kuwa kampuni hiyo ililipwa na Jubilee ili kukiunda upya wakati wa kampeni za 2017.

Cambridge Analytica inahusishwa na ushindi wa urais wa Donald Trump nchini Marekani. Facebook kwa upande wake iliwaomba watumiaji wake radhi na kusema imeweka mikakati ya kuhakikisha habari za wateja wake hazidukuliwi tena.

Habari Hii Imenakiliwa Kupitia SwahiliHub

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

Pata Habari za Teknolojia Kupita Barua Pepe

By pressing the Subscribe button, you confirm that you have read and are agreeing to our Privacy Policy and Terms of Use