in

Je Wajua Google Inarekodi Maongezi Yako Bila Wewe Kujua

Na hivi ndivyo Google inavyofanya kurekodi maongezi yako

Je Wajua Google Inarekodi Maongezi Yako Bila Wewe Kujua

Sababu siku ya jumapili tulikuwa kwenye uzinduzi wa Samsung Galaxy S9 na hatukuweza kuwaletea makala ya JeWajua, leo nimeona niwaletee hii kama kulipiza makala ya jumapili iliyopita.

Sasa leo nimekuja na makala hii ambayo najua itakuwa ni kitu cha kushangaza kidogo kwa watu mbalimbali hasa wale ambao ni wataalam sana wa kutumia teknolojia. Ukweli ni kuwa wakati mwingine kuwa mjuzi sana hasa wa maswala haya ya Teknolojia ndio chanzo cha wewe kuweza kuharibu maisha yako kwa namna moja ama nyingine.

Najua hapa utakuwa unajiuliza ni kwanini nasema hivi, na ili kujua naomba uwe na subira na uwe na mimi mpaka mwisho wa makala hii. Kama kichwa cha habari ya makala hii kinavyosema leo ninaenda kukuonyesha jinsi Google inavyo rekodi maongezi yako kutoka kwenye simu yako ya Android bila hata wewe kujua.

Sehemu inayotumika kurekodi mazungumzo yako kwenye simu ni sehemu maarufu sana kwa wataalam wa teknolojia yaani sehemu ya Google Assistant. Kwa wale ambao hawajui kuhusu Google Assistant hii ni sehemu ambayo unaweza kuongea nayo kupitia simu yako Android. Sehemu hii inaweza kufanya mambo mbalimbali kwenye simu yako kama kuchukua picha ya simu yako (screenshot) pale utakapo hitaji, kutafuta kitu kwenye Google, pamoja na mambo mengine mengi. Kama unataka kujua zaidi Kuhusu Google Assistant basi soma kwenye ukurasa huu.

Sasa sehemu hii huwashwa kwa kusema maneno kama “Ok Google” au “Hey Google” na Maneno haya hutegemewa kufanya kazi endapo ni sauti yako imesikika ikisema maneno hayo na sio vingenevyo. Sasa kuna wakati sehemu hii hufanya kazi bila hata wewe kusema maneno hayo sasa kama unatumia sehemu ya Google Assistant unaweza kutembelea ukurasa huu kwenye kisakuzi chako cha Chrome history.google.com.

Kisha baada ya kuingia angalia upande wa kushoto chagua sehemu iliyo andikwa Activity Control, kisha shuka mpaka chini kidogo utaona sehemu iliyo andikwa Voice & Audio Activity kisha bofya sehemu iliyo andikwa kwa herufu kubwa MANAGE ACTIVITY, Sasa hapo utaona list ya audio zote ulizokuwa unaongea na sehemu ya Google Assistant, Ndani ya audio hizo utagundua kuna audio zingine ulikua hata uongei na Sehemu ya Google Assistant yaani hukuwa umewasha sehemu hiyo kwa kusema maneno ya “Ok Google” au “Hey Google”.

Sasa tunakuja kwenye sababu kwanini ninasema wakati mwingine kuwa mjuzi sana wa mambo hasa ya teknolojia sio kitu kizuri sana. Sababu ni kuwa sehemu hii ya Google Assistant huwa imezimwa unapo nunua simu ya Android, watu wasio jua kuhusu mambo ya teknolojia na uhakika mpaka sasa hawajui kuhusu sehemu hii na inawezekana hujui hata kama sehemu hii ipo kwenye simu yako. Hivyo unakuta unajiepusha na mambo kama haya ya kurekodiwa kwa sababu tu hukujua kuhusu uwepo wa sehemu hiyo ya Google Assistant kwenye simu yako.

Ukweli ni kuwa teknolojia ni ya watu wengi na huwezi kuizuia hivyo ni muhimu kuizuia kwa upande wako binafsi, yaani sehemu kama hizi za kurekodi mambo yako binafsi zipo sana na nyingine zipo kwenye programu mbalimbali ambazo inawezekana unatumia sasa kwenye simu yako, ndio maana nakwambia teknolojia ni ya watu wengi kwa sababu huwezi kuizuia endapo unatumia teknolojia tena kwa ukamilifu. Kwenye simu yako unakuta unayo kila programu bila kujua pengine programu hizi zinauwezo wa kufanya kazi nyuma ya pazia.

Sasa ushauri wangu ni kuwa unaweza kudhibiti matumizi yako ya programu mbalimbali kwenye simu yako tena hasa zile ambazo hutumii na tumia programu ambazo unajua zinakupa msaada kwenye maisha yako ya kila siku. Pia ni muhimu kusoma vigezo na masharti pamoja na sera ya faragha kabla ya kutumia programu yoyote hii itakusaidia kujua ni kitu gani kina chukuliwa na kuhifadhi na watengenezaji wa programu husika.

Written by Amani Joseph

Tanzania Tech tumejikita kuhakikisha hupitwi na habari yoyote ya teknolojia, endelea kuwa nasi tufuate kwenye mitandao ya kijamii.

Toa Maoni Hapa

Kumbuka ni Muhimu Kuandika Jina Halisi na Barua Pepe, Vigezo na Masharti Kuzingatiwa.

6 Comments